Mamlaka
ya Hali ya Hewa nchini Tanzania –TMA imesema katika msimu wa mvua za Novemba
2024 mpaka April 2025 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika
maeneo mengi ya kanda za Magharibi.
Imesema
mvua hizo ni mahususi kwa mikoa inayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka kanda
ya magharibi,kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa
pwani ya kusini pamoja na maeneo yaliyopo kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Hayo
yameelezwa jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya
Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a wakati
akitoa mwelekeo wa msimu wa mvua Novemba 2024 mpaka
April 2025.
‘Aidha,
kwa maeneo ya kanda ya Ziwa Victoria mvua zilitarajiwa kuwa za Wastani hadi
Chini ya Wastani. Msimu wa Vuli, 2024 ulitarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya
ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha. Aidha, mvua hizo zilitarajiwa kuanza
kwa kusuasua wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024 katika ukanda wa Ziwa Victoria
na kusambaa katika maeneo mengine yanayopata mvua za Vuli kati ya wiki ya pili
na ya tatu ya mwezi Oktoba, 2024’amesema Dkt Chang’a
Aidha
Dkt Chang’a amesema katika msimu huo Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja
na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao kwa maeneo
yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani.
Amewashauri
Wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa
kuzingatia hali ya unyevu katika udongo, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia
maji kutuama shambani, kuhifadhi maji shambani, kuzuia mmomonyoko na upotevu wa
rutuba kutokana na kutuwamisha maji kwa muda mrefu au mafuriko.
Awali
akitoa tathmini ya mvua za msimu uliopita Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka
Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) Rose Senyagwa amesema maeneo mengi
yanayopata mvua za msimu mmoja kwa mwaka yalipata mvua za juu ya wastani
isipokuwa maeneo machache.
Hata hivyo Mamlaka hiyo imewashauri wadau wa Sekta Binafsi kushirikiana na wataalamu mbalimbali ikiwemo wataalam wa hali ya hewa ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza katika wakati huo wa msimu wa mvua.

Chapisha Maoni